Zaburi Sura 64
1
Mungu, uisikie sauti yangu katika malalamiko yangu; Unilinde uhai wangu na hofu ya adui.
2
Utanificha mbali na shauri la siri la watenda mabaya, Mbali na ghasia ya watu wafanyao maovu;
3
Waliounoa ulimi wao kama upanga, Wameielekeza mishale yao, maneno ya uchungu,
4
Wapate kumpiga mkamilifu faraghani, Kwa ghafula humpiga wala hawaogopi.
5
Walijifanya hodari katika jambo baya; Hushauriana juu ya kutega mitego; Husema, Ni nani atakayeiona?
6
Hutunga maovu; husema, Tumefanya shauri kamili; Na mawazo ya ndani ya kila mmoja wao, Na moyo wake, huwa siri kabisa.
7
Kwa hiyo Mungu atawapiga shabaha, Kwa mshale mara watapigwa.
8
Ndivyo watakavyokwazwa, Ulimi wao wenyewe ukishindana nao. Wote wawaonao watatikisa kichwa.
9
Na watu wote wataogopa, Wataitangaza kazi ya Mungu, Na kuyafahamu matendo yake.
10
Mwenye haki atamfurahia Bwana na kumkimbilia, Na wote wenye moyo wa adili watajisifu.