Zaburi Sura 63
1
Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku, Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.
2
Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu, Nizione nguvu zako na utukufu wako.
3
Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai; Midomo yangu itakusifu.
4
Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai; Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.
5
Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono; Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha.
6
Ninapokukumbuka kitandani mwangu, Nakutafakari Wewe makesha yote ya usiku.
7
Maana Wewe umekuwa msaada wangu, Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia.
8
Nafsi yangu inakuandama sana; Mkono wako wa kuume unanitegemeza.
9
Bali waitafutao nafsi yangu, ili kuiharibu, Wataingia pande za nchi zilizo chini.
10
Watatolewa wafe kwa nguvu za upanga, Watakuwa riziki za mbwa-mwitu.
11
Bali mfalme atamfurahia Mungu, Kila aapaye kwa Yeye atashangilia, Kwa maana vinywa vya waongo vitafumbwa.