Zaburi Sura 112
1
Haleluya. Heri mtu yule amchaye Bwana, Apendezwaye sana na maagizo yake.
2
Wazao wake watakuwa hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
3
Nyumbani mwake mna utajiri na mali, Na haki yake yakaa milele.
4
Nuru huwazukia wenye adili gizani; Ana fadhili na huruma na haki.
5
Heri atendaye fadhili na kukopesha; Atengenezaye mambo yake kwa haki.
6
Kwa maana hataondoshwa kamwe; Mwenye haki atakumbukwa milele.
7
Hataogopa habari mbaya; Moyo wake u imara ukimtumaini Bwana.
8
Moyo wake umethibitika hataogopa, Hata awaone watesi wake wameshindwa.
9
Amekirimu, na kuwapa maskini, Haki yake yakaa milele, Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu.
10
Asiye haki ataona na kusikitika, Atasaga meno yake na kuyeyuka, Tamaa ya wasio haki itapotea.