Zaburi Sura 56
1
Mungu, unirehemu, maana yuko atakaye kunimeza, Mchana kutwa ananionea akileta vita.
2
Adui zangu wanataka kunimeza mchana kutwa, Maana waletao vita juu yangu kwa kiburi ni wengi.
3
Siku ya hofu yangu nitakutumaini Wewe;
4
Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwenye mwili atanitenda nini?
5
Mchana kutwa wanapotosha maneno yangu, Mawazo yao yote ni juu yangu kunitakia mabaya.
6
Hukutanika, hujificha, huziangalia nyayo zangu, Kwa kuwa wameniotea nafsi yangu.
7
Je! Wataokoka kwa uovu wao? Ee Mungu, uwaangamize kwa hasira yako.
8
Umehesabu kutanga-tanga kwangu; Uyatie machozi yangu katika chupa yako; (Je! Hayamo katika kitabu chako?)
9
Ndipo adui zangu watarudi nyuma siku ile niitapo. Neno hili najua kuwa MUNGU yu upande wangu;
10
Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Kwa msaada wa Bwana nitalisifu neno lake.
11
Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?
12
Ee Mungu, nadhiri zako zi juu yangu; Nitakutolea dhabihu za kushukuru.
13
Maana umeniponya nafsi yangu na mauti; Je! Hukuizuia miguu yangu isianguke? Ili nienende mbele za Mungu Katika nuru ya walio hai.