Zaburi Sura 141
1
Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo.
2
Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.
3
Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.
4
Usiuelekeze moyo wangu kunako jambo baya, Nisiyazoelee matendo yasiyofaa, Pamoja na watu watendao maovu; Wala nisile vyakula vyao vya anasa.
5
Mwenye haki na anipige, itakuwa fadhili; Anikemee, itakuwa kama mafuta kichwani; Kichwa changu kisikatae, Maana siachi kusali kati ya mabaya yao.
6
Makadhi wao wakiangushwa kando ya genge, Watayasikia maneno yangu, maana ni matamu.
7
Kama kupasua kuni na kuzichanja juu ya nchi, Ndivyo ilivyo mifupa yetu mdomoni pa kuzimu.
8
Macho yangu yanakuelekea Wewe, MUNGU Bwana, Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu.
9
Unilinde na mtego walionitegea, Na matanzi yao watendao maovu.
10
Wabaya na waanguke katika nyavu zao wenyewe, Pindi mimi ninapopita salama.