Ayubu Sura 23
1
Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,
2
Hata leo mashitaka yangu yana uchungu; Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu.
3
Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona, Nifike hata hapo anapokaa!
4
Ningeiweka daawa yangu mbele yake, Na kukijaza kinywa changu hoja.
5
Ningeyajua maneno atakayonijibu, Na kuelewa na hayo atakayoniambia.
6
Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake? La, lakini angenisikiliza.
7
Hapo walekevu wangepata kuhojiana naye; Basi hivyo ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele.
8
Tazama, naenda mbele, wala hayuko; Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona;
9
Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona; Hujificha upande wa kuume, hata nisimwone.
10
Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.
11
Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka.
12
Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,
13
Lakini yeye ni mmoja, ni nani awezaye kumgeuza? Tena nafsi yake ilitakalo, ndilo afanyalo.
14
Kwani yeye hulitimiliza hilo nililoamuriwa; Tena mambo mengi kama hayo ya pamoja naye.
15
Kwa hiyo naona taabu mbele ya uso wake; Nitakapofikiri, namwogopa.
16
Kwani Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia, Naye Mwenyezi amenitaabisha;
17
Maana sikufadhaishwa kwa sababu ya giza, Wala kwa sababu giza kuu limenifunika uso.