Zaburi Sura 150
1
Haleluya. Msifuni Mungu katika patakatifu pake; Msifuni katika anga la uweza wake.
2
Msifuni kwa matendo yake makuu; Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.
3
Msifuni kwa mvumo wa baragumu; Msifuni kwa kinanda na kinubi;
4
Msifuni kwa matari na kucheza; Msifuni kwa zeze na filimbi;
5
Msifuni kwa matoazi yaliayo; Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.
6
Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana. Haleluya.